SIKU YA KUTAWAZWA IMAM ALI IBN ABU TALIB (AS) KUWA KIONGOZI WA WAUMINI.



Tukio la Ghadeer Khum la kutawazwa kwa Imam Ali Ibn Abu Talib (as) kuwa Mrithi halali wa Mtume (saww) na kuwa kiongozi wa Waislam imeandikwa na wanazuoni wengi wakiwemo wa Ahlu Sunnah ambao wameandika katika vitabu vifuatavyo:: Tafsirul Kabiir, juz 12, uk 49

: Tafsirun Naysabury, juz 6, uk 194

: Al Isaba, juz 1, uk 305

: Tarekh Baghdad, juz 8, uk 290

: Ihqaaqul Haqqi, juz 6, uk 225-304

: Al Mirqatu fiy Sharhil Mishkaat, juz 5, uk 574

: Tafsirul Basair, juz 49, uk 7

: Tafsirul Qurtubi, juz 18, uk 278

: Ruuhul Maany, juz 29, uk 404

: Manaqibul Imam Ali (as), uk 23

: Sharhu Nahjul Balagha, juz 4, uk 74

: Addurrul Manthur, juz 2, uk 107

: Sahih Muslim, juz 4, uk 1873

: Na zingine nyingi

Baada ya kumaliza Hijja, Mtume Muhammad (saww) akiwa amefuatana na maswahaba wake waliofikia 120,000 wakiwa wanarudi kwenye miji yao walifika eneo linaitwa Ghadeer Khumm ambapo palikuwa na bonde iliyokuwa ina chemchem ya maji na mahala hapo ndipo palikuwa na njia panda za kuelekea miji tofauti.

Wasafiri wengi walikuwa wanatumia njia hiyo ili kuchota maji na kuendelea na safari zao.

Msafara huo wa Mtume (saww) na maswahaba waliokuwa wanarudi Hijja walifika mahala hapo tarekhe 18 Dhul Hijja, mwaka wa 10 Hijriyya.Wakati Mtume (saww) alipofika hapo, Mwenyezi Mungu Akamshushia Aya ya 67 ya Sura ya 5 Akisema:

Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako, na kama hukufanya, basi hukufikisha Ujumbe Wake.Na Mwenyezi Mungu Atakulinda na watu, hakika Mwenyezi Mungu Hawaongozi watu makafiri. 



1. Ni jambo gani ambalo Mwenyezi Mungu Alimtaka Mtume wake (saww) alifikishe kwa watu hao ambao walikuwa ni mkusanyiko wa Waislamu wengi waliokutana kwa pamoja na sehemu moja?

2. Ni ujumbe gani huo ambao kama Mtume Muhammad (saww) hakulifikisha, basi itakuwa ni sawa na kuwa hakufikisha ujumbe wowote katika miaka yake yote ya Utume?

3. Ni ujumbe gani huo ambao Mtume (saww) alikuwa anatakiwa alifikishe bila ya kuwaogopa watu na kwamba Mwenyezi Mungu Atamlinda na makafiri?

4. Je! Palikuwepo na makafiri katika huo mkumbo wa watu 120,000 ambao walikuwa wanatoka kufanya Hijja?

Baada ya kupokea Aya hiyo, Mtume (saww) akawaagiza watu wasitawanyike, na wale waliokwisha kuondoka wakaitwe warudi mahala hapo na kuwangoja wale ambao walikuwa bado hawajafika pale. Mtume (saww) akaagiza itengenezwe Mimbar, watu wakasema hapa hakuna mbao wala mili ya kutengenezea Mimbar!Mtume (saww) akaagiza watu watumie matandiko ya ngamia na farasi wao kutengeneza Mimbar.

Baada ya Mimbar kuwa tayari na watu wote kukusanyika, Mtume (saww) akatoa khutba ndefu akikumbusha sheria za Uislam, mambo ya Sala, kutoa Zaka na mengineyo.

Mwishoni Mtume (saww) akawasomea Aya ya 67 aliyoipokea hapo, kisha akawauliza watu; Je! Katika watu, ni nani aliye bora zaidi kwa waumini kuliko nafsi zao?Watu wote kwa pamoja wakasema; Ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wajuao.

Hapo Mtume (saww) akamuita Imam Ali Ibn Abu Talib (as) na kumtaka apande juu ya ile Mimbar, kisha akaushika mkono wa Ali (as) akauinua juu kabisa kisha Mtume (saww) akasema: Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Kiongozi wangu, na Mimi ni Kiongozi wa Waumini, na Mimi ni bora zaidi kuliko nafsi zao, kisha akasema: Ambaye mimi ni Kiongozi wake, basi huyu Ali ni Kiongozi wake. Ee Mola! Muunge atakaemuunga Ali na Mtenge atakaemtenga Ali!  

Mtume (saww) alisema “Man Kuntu Mawlahu, fa haadha Aliyyun Mawlahu”.Watu wengi ambao wanajiita kuwa ni Waislam wanasema kuwa Mtume (saww) alitumia neno la Mawla akiwa anamaanisha kuwa ni Rafiki, Yaani kwa kila ambaye mimi ni Rafiki wake, basi Ali (as) ni Rafiki yake!


Sasa hebu tuichambue neno Mawla lina maana ipi katika Qur’aan Tukufu.
Neno “Mawla” lina maana (tafsiri) 10 lakini nitatoa mifano minne kutoka kwenye Qur’aan Tukufu:

: Rafiki; Katika Sura ya 57, Aya ya 15, Moto wa Jehannam imeitwa Mawla (Rafiki) wa waliokufuru.

: Bwana; Katika Sura ya 16, Aya ya 76, Mmiliki wa mtumwa ameitwa Mawla (bwana).

: Mlinzi; Katika Sura ya 47, Aya ya 11, Mwenyezi Mungu Ameitwa Mawla (mlinzi).

: Imam/Kiongozi: Katika Sura ya 33, Aya ya 6, Mwenyezi Mungu Amemuita Mtume kuwa Awla. 

Sasa tuulizane, Mtume aliposema ambaye mimi ni Mawla wake, basi Ali (as) ni Mawla wake, alikuwa anamaanisha nini?Kama alikuwa anamaanisha kuwa ni Rafiki, hebu tuulizane Mtume (saww) alikuwa na marafiki wangapi?

Na iweje Mwenyezi Mungu Amuamrishe Mtume (saww) awazuie Waislam mahala pale eti kwa ajili ya kumtambulisha Imam Ali (as) kuwa ni Rafiki wa Mtume (saww) na ni rafiki wa kila ambaye ni rafiki wa Mtume (saww)?

Je! Huo ndio ujumbe makhsusi ambao Mwenyezi Mungu alitaka Mtume (saww) aufikishe na kama hakuufikisha basi atakuwa hajafanya lolote kufikisha ujumbe wa Mwenyezi Mungu?

Je! Ni kwanini Mtume (saww) aogope kufikisha ujumbe wa kusema Ambaye mimi ni rafiki wake basi Ali (as) ni rafiki wake?Kwani kulikuwa na jambo gani la kuogopesha hapo?Itikadi hiyo na mawazo hayo ni ya kupotoka na ya kupotosha!

Ukweli ni kuwa Mtume (saww) alikuwa anahofilia kumtaja Imam Ali (as) kuwa ni Mrithi wake baada ya kufariki kwake kwa kuwa alikuwa anawajua maadui ambao walikuwa wanamchukia Imam Ali (as) na ambao walikuwa tayari kumdhuru Imam Ali (as) ambao walikuwa wamejivika maguo ya Uislam lakini walikuwa ni makafiri na wanafik!

Ujumbe huo wa kumtawaza Imam Ali Ibn Abu Talib (as) ndio ulikuwa wa muhimu sana kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwa kila Nabii alikuwa anamtaja Mrithi wake kabla ya yeye kufariki au kuuawa.

Baada ya kumaliza zoezi hilo la kumtawaza Imam Ali (as), ikafuata zoezi la watu wote waliokuwepo pale kumpa mkono wa Baiyya (kukubali) kuwa Imam Ali (as) ni kiongozi wao baada ya Mtume (saww).

Wanaume wakawa wanampa mkono Imam Ali (as), na ilipofikia zamu ya wanawake, likachukuliwa sufuria yenye maji kisha Imam Ali (as) akaweka mikono ndani mwake halafu wanawake wakawa wanaweka mikono yao ndani ya lile sufuria.

WALIOANGAMIA BAADA YA KUVUNJA BAIYYA ZAO KWA IMAM ALI (AS)

Mtu mmoja aitwae Harith bin Nuuman Alfihri alitoa maneno ya kejeli kwa Mtume (saww) kwa kusema: Umetuagiza tusali, tutoe zaka, tufanye Hijja na mengineyo mengi, sasa unatuagiza tumfanye nduguyo Ali kuwa kiongozi wetu, je hayo ni maagizo ya Mwenyezi Mungu au ni amri yako binafsi?

Kama ni maagizo ya Mwenyezi Mungu, basi nataka anidondoshee adhabu sasa hivi!Pale pale alidondokewa na jiwe kutoka mbinguni na akafa pale pale!

Muulizaji aliuliza juu ya adhabu itakayotokea juu ya makafiri, hapana awezaye kuizuia. (Qur’aan 70:1-2)Maswahaba wengine Zayd bin Arqam na Anas bin Malik wao baadaye walitengua viapo vyao vya utiifu kwa Imam Ali (as), wao walifikiwa na balaa kubwa, Zayd alipofuka macho na Anas bin Malik alipata ukoma.

YALIYOTOKEA BAADA YA TUKIO LA KUTAWAZWA IMAM ALI IBN ABU TALIB (AS)

Baada ya kumalizika zoezi la kutawalishwa Imam Ali (as) na watu kumpa baiyya ya utiifu, Mwenyezi Mungu Akashusha Aya ya 3, Sura ya 5 ikisema:Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na kukutimizieni Neema Yangu, na Nimekupendeleeni Uislam uwe Dini Yenu.

Mutaona kuwa Aya hii imepangiliwa katika Qur’aan katika Sura Maidah kuwa ni ya 3 wakati Aya hii ndiyo ilikuwa ya mwisho kabisa ya Qur’aan baada ya tukio la Ghadeer Khum ikitanguliwa na Aya ya 67 ya Sura ya Maidah.Baada ya Sura ya 3 kushushwa, hapakushuka Aya yoyote ya Qur’aan.

Hata hivyo sehemu hiyo ya Leo Nimekukamilishieni Dini Yenu imeingizwa katika hiyo Aya ya 3 ili kupoteza ukweli kuwa Aya hiyo ilikuwa ndiyo ya Mwisho kabisa kushushushwa!

Nawatakia Waumini wote Kheri, Baraka na Furaha katika siku hii tukufu ya EID UL GHADEER.

AMEEN.

Comments