"TUMTANGULIZE MUNGU KWA KILA JAMBO" SHEIKH JALALA

 

Mkuu wa Chuo cha Imam Swadiq (a.s) na Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Ithna'ashariyyah Tanzania-TIC Maulana Sheikh Hemedi Jalala amewataka Waislamu na Watanzania kuwa na tabia ya kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika kila jambo kama alivyokuwa anafanya Imam Khomein (R.A) katika maisha yake.

Sheikh Jalala amesema hayo jana katika maadhimisho ya kumbukizi ya Kifo cha Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Imam Khomein, yaliyofanyika katika ukumbi ya TIC Makao Makuu Kigogo, Dar es Salaam.

"Tunakumbuka kifo cha Mwanachuoni mkubwa, kifo cha mtu wa Mungu mkubwa, kifo cha mpenda Amani mkubwa Ayatullah Imam Khomein (r.a), ukisoma maisha yake utampata kwenye kila jambo lake alimtanguliza Mwenyezi Mungu, kwenye kila kitu chake Mwenyezi Mungu ndie alikuwa mstari wa mbele. na mimi naamini dunia ya leo kwenye mabadiliko mengi yameyotokea, ikiwemo na mmomonyoko wa maadili, tunahitajia kumtanguliza Mwenyezi Mungu katika mambo yetu" alisema Sheikh Jalala

 Maadhimisho hayo yalihudhuirwa na Viongozi wa Dini mbalimbali akiwemo Sheikh Hamis Nasoro Mwenyekiti wa Umoja wa Maimamu Chalinze – Pwani na Mchungaji Kiame Naibu Mwenyekiti Umoja wa Makanisa Mkoa Dar es Salaam.

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, sawa na tarehe 14 Khordad mwaka 1368 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia sawa na mwezi Juni 1989, Imam Ruhullah Musawi Khomeini (M.A) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87. Ulimwengu wa Kiislamu uligubikwa na majonzi na huzuni kubwa kuutokana na kutangazwa kifo cha Imam.

Imam Khomeini (M.A) alizaliwa tarehe Mosi mwezi wa Mehr mwaka 1281 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 24 Septemba 1902 katika mji wa Khomein ulioko katikati mwa Iran. Alianza kujishughulisha na siasa sambamba na masuala ya kielimu na kiutamaduni. Mapambano ya Imam dhidi ya utawala wa Shah na uingiliaji wa Marekani nchini Iran yalishtadi mwaka 1963 Milaadia sawa na 1342 kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, na kupelekea Imam kubaidishwa kwa miaka 13 nchini Iraq, Uturuki na Ufaransa. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipata ushindi mwaka 1357 Hijiria Shamsia sawa na tarehe 1979 kwa uongozi shupavu wa Imam Khomeini (M.A).








Comments