Rais wa Palestina autaka Umoja wa Mataifa usimamishe uwanachama wa Israel

 


Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameuhimiza Umoja wa Mataifa usimamishe uwanachama wa utawala haramu wa Israel katika chombo hicho kikuu cha dunia mpaka utakapokomesha uchokozi na ukandamizaji wake dhidi ya Wapalestina na kutekeleza maazimio ya Umoja wa Mataifa ya uundaji mataifa mawili tofauti ya Israel na Palestina na kutekelezwa haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurejea makwao.

Abbas alitoa mwito huo jana Jumatatu wakati wa maadhimisho ya kwanza rasmi kufanywa na Umoja wa Mataifa ya "Siku ya Nakba" ya maafa ya kuhamishwa kwa nguvu mamia kwa maelfu ya Wapalestina kutoka eneo ambalo sasa linaitwa Israel wakati wa machafuko ya kugawanywa ardhi ya Palestina miaka 75 iliyopita.

Zaidi ya Wapalestina 760,000 walikimbia au walifukuzwa kutoka makwao mnamo 1948 wakati utawala bandia wa Israel ulipoundwa, tukio ambalo Wapalestina wanaliita Nakba - au janga - na kuadhimishwa kila mwaka Mei 15.

Katika hotuba iliyojaa hisia za hamasa aliyotoa kwa muda wa saa nzima, Abbas aliuliza mataifa ya dunia kwa nini zaidi ya maazimio 1,000 yaliyopitishwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhusu Wapalestina hayajawahi kutekelezwa.

"Tunadai leo rasmi, kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio ya kimataifa, kuhakikisha kuwa Israel inaheshimu maazimio haya au kusimamishwa uanachama wa Israel katika Umoja wa Mataifa", alisisitiza rais huyo wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina.

Umoja wa Mataifa unaadhimisha kumbukumbu ya Nakba katika makao yake makuu mjini New York mwaka huu kwa mara ya kwanza baada ya azimio la kuadhimisha siku hiyo kupitishwa mwezi Novemba mwaka jana.

Katika taarifa yake Jumatatu, Rosemary DiCarlo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kisiasa na kujenga amani alisema, Wapalestina wanastahili maisha ya haki na utu na kutekelezewa haki yao ya kujitawala na kujitegemea.

Kupitia mitandao ya kijamii, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa pia zimeonyesha mshikamano na uungaji mkono wao kwa watu wa Palestina na piganio lao tukufu la kujikomboa na kuunda nchi yao...


Comments