Mufti wa Yemen ametangaza mshikamano na wananchi na Muqawama wa Palestina na akasisitiza kuwa, haifai kunyamazia kimya na kufumbia macho matukio ya Ulimwengu wa Kiislamu hususan Palestina.
Siku ya Jumanne asubuhi ya tarehe 9 Mei, jeshi la utawala
haramu wa Kizayuni wa Israel lilianzisha operesheni mpya ya hujuma na
mashambulio ya kijeshi liliyoiita "Ngao na Mshale" dhidi ya Ukanda wa
Gaza, ambapo Wapalestina 35 waliuawa shahidi na wengine wasiopungua 150
walijeruhiwa.
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen jana Jumapili walijitokeza
barabarani kuonyesha mshikamano na uungaji mkono kwa Wapalestina wa
Ukanda wa Gaza na kutoa nara dhidi ya utawala wa Kizayuni. Mikusanyiko
na maandamano hayo ya jana yalifanyika kwa anuani ya "Masira
Tha'arul-Ahrar" (Maandamano ya Kisasi cha Watu Huru) ili kuonyesha
mshikamano na uungaji mkono kwa Palestina.
Jana jioni pia ulifanyika mkusanyiko mkubwa katika miji ya Sana'a
na Hudaidah, ambapo watu wengi kutoka maeneo ya jirani ya mji mkuu wa
Yemen Sana'a walihudhuria katika mkusanyiko huo.

Kwa mujibu wa chaneli ya habari ya Al-Masirah, Mufti wa Yemen Sheikh Shamsuddin Sharafuddin alisisitiza katika mkusanyiko huo: "tunatangaza mshikamano na ndugu zetu mujahidina huko Palestina na tunasisitiza kuwa tunawaunga mkono na kamwe hatutawaacha ndugu zetu wa Palestina peke yao".
Mufti wa Yemen amefafanua kwa kusema: "sisi taifa la Yemen ni watu
tuliokomboka, na msimamo wetu wa kila siku ni kuunga mkono masuala ya
Waislamu, la kwanza kabisa likiwa ni Palestina na Quds Tukufu. Vile vile
tunautaka Umma wa Kiislamu uziunganishe pamoja medani za mapambano".
Aidha, Mufti wa Yemen amesema nchi za Kiarabu na Kiislamu
zilizofanya mapatano na suluhu na Tel Aviv ndizo zinazobeba dhima ya
uchokozi wa kila mara linaofanyiwa taifa la Palestina na akasisitiza
kuwa: kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu ni haramu na wale
wanaoshiriki katika mikutano ya adui si wawakilishi wa umma wa Kiarabu
na Kiislamu.../
Comments
Post a Comment