Hizbullah yafanya mazoezi ya kijeshi kusini ya Lebanon ya kujiandaa na vita na Israel

 


Vikosi vya wanamuqawama wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon vimefanya mazoezi maalumu ya kijeshi katika moja ya kambi za harakati hiyo kusini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, katika mazoezi hayo ya kijeshi vikosi vya wanamapambano wa Hizbullah vimefanya mazoezi ya kushabihisha vita vinavyoweza kutokea baina yao na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Katika manuva hayo, vikosi vya wanamuqawama wa Hizbullah vimetumia zana za kivita, baadhi ya vifaa vya kijeshi ikiwa ni pamoja na makombora ya kutungulia vifaru, bunduki za udunguaji pamoja na mizinga.

Ustadi wa kupambana kivita mtu mmoja mmoja, nao pia umeonyeshwa katika mazoezi hayo ya kijeshi ya Hizbullah. Kilichotoa mguso zaidi katika manuva hayo ya harakati ya muqawama ya Hizbullah ni utumiaji wa ndege zisizo na rubani za droni ambazo zitaweza kutumika katika vita vyovyote vile ambavyo vinaweza kutokea katika siku za usoni.

Ndege hizo zisizo na rubani zimepaa katika anga ya kusini mwa Lebanon na kufuatilia harakati na nyendo za wanajeshi wa Israel katika vita mshabaha baina ya utawala huo haramu na Lebanon.

Aidha, bendera za Lebanon na Hizbullah zimepeperushwa angani na ndege zisizo na rubani za Muqawama wa Kiislamu kusini mwa nchi hiyo.

Utumiaji wa ndege zisizo na rubani katika mazoezi ya kijeshi ya Hizbullah kumetuma ujumbe kwamba Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon umepiga hatua kubwa za ustawi katika sekta ya kijeshi...

Comments